MAKONGORO Mahanga, amesema sera ya kodi, fedha, uchumi na uwekezaji katika serikali ya awamu ya tano zina walakini mkubwa na kwamba ndiyo chanzo cha hali mbaya ya kiuchumi hapa nchini ikiwemo kuadimika kwa fedha mikono mwa wananchi, anaandika Pendo Omary.
Dk. Mahanga alikuwa Naibu Waziri Wizara ya Kazi na Ajira katika serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete na pia alikuwa Mbunge wa Jimbo la Segerea kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (2005-2015), kabla ya kuhamia Chadema mwaka Agosti mwaka huu.
Akizungumza na MwanaHALISI Online leo, Mahanga ambaye ni mtaalamu wa mambo ya fedha na uchumi amesema ukusanyaji wa kodi ni jambo jema, ila lazima lifanywe kwa kujali maslahi ya wawekezaji na wafanyabiashara ambao ndiyo walipa kodi na waajiri.
“Serikali inaangalia zaidi kukusanya mapato yake bila kujali sana mazingira wezeshi ya wafanyabiashara na wawekezaji ambao ndio walipa kodi. Kwa kifupi sera na taratibu za kodi na ukusanyaji wake unaua sekta binafsi ambayo ndiyo injini ya maendeleo,” amesema Dk. Mahanga.
Ameongeza kuwa “hata uamuzi wa Serikali kuzuia sekta binafsi kufanya biashara na Serikali ni uamuzi mbaya sana. Utaua sekta binafsi na kupoteza ajira nyingi sana za watanzania kwani Sekta binafsi wanaponyimwa kabisa fursa za kupata kandarasi za serikali, watakosa biashara, sasa kodi ya kutosha watalipaje?”
Dk. Mahanga amesema kwa maoni yake sera ya kodi, fedha, uchumi na uwekezaji zina walakini mkubwa na maamuzi ya kisiasa yasiyozingatia utashi wa kitaalamu ndiyo umeifikisha nchi katika hali mbaya ya uchumi na mzunguko wa fedha kwa wananchi kuwa mdogo.
Pia ameonya kuwa, maamuzi ya baadhi ya matumizi ya serikali kufanyiwa Ikulu badala ya bungeni ni kuvunja Katiba na misingi ya utawala bora.
“Ununuzi wa ndege ili kufufua shirika la ndege hapa nchini ni mzuri lakini hazikupaswa kununuliwa ndege nyingi mfululizo na bila kufuata vipaumbele vya maendeleo ya nchi,” amesema.