Wednesday, January 4, 2017

WAZIRI MKUU AFUTA POSHO NA KUWAPA SIKU TATU WATUMISHI AMBAO HAWAJALIPOTI KIGAMBONI#johnleo

*WAZIRI MKUU AFUTA POSHO NA KUWAPA SIKU TATU WATUMISHI AMBAO HAWAJARIPOTI KIGAMBONI.*

*Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa, leo tarehe 3/1/2017 amefanya ziara ya kikazi wilaya ya Kigamboni.*

*Waziri Mkuu amezungumza na watumishi wa Halmashauri ya manispaa Kigamboni na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na kuepuka vitendo vya urasimu na rushwa.*

*Amewapongeza Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Mhe Hashim Mgandilwa na Mkurugenzi wa manispaa ya Kigamboni Ndg Stephen Katemba kwa jinsi wanavyosimamia Wilaya na Halmashauri ya manispaa na kuhakikisha huduma zenye tija zinapatikana katika kuwahudumia wananchi licha ya muda mfupi tangu kuanzishwa kwa wilaya hii.*

*Pia Waziri Mkuu amewapa siku tatu tu watumishi kumi ambao walitakiwa kuhamia Kigamboni wakitokea Temeke kufanya hivyo mara moja na endapo hawatahamia ndani ya muda huo watafukuzwa kazi.*

*Akizungumzia suala la kubana matumizi, Waziri Mkuu amesema kuwa posho zote ambazo zinatengwa kwa ajili ya mapochopocho maofisini (Bites Allowance) zifutwe na badala yake pesa hizo zielekezwe katika miradi ya maendeleo. Amesisitiza kuwa hili ni agizo kwa manispaa zote za Mkoa wa Dar es salaam.*

*Mapema akiwasilisha taarifa ya Wilaya ya Kigamboni, Mkuu wa wilaya hiyo Mhe Hashim Mgandilwa pamoja na mambo mengine, amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa wamejipanga kuleta maendeleo na kumuomba Waziri Mkuu kuingilia kati suala la KDA (Kigamboni Development Agency) ili kuacha ardhi ya Kigamboni isimamiwe na mamlaka moja ya Halmashauri ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi.*

*_"......KDA imekuwa ikisuasua na kusababisha migogoro, naomba mamlaka ya usimamizi wa ardhi ya Kigamboni ibakie kwa halmashauri ili kuharakisha maendeleo...., sisi Kigamboni tumejipanga, tunataka kuupanga mji wetu kuwa wa mfano uliopangika na unaovutia kuliko wilaya zote za Mkoa wa Dar es salaam....._"* DC Mgandilwa alisisitiza.

*Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezindua wodi ya uzazi ya akina mama katika Zahanati ya Kisarawe II iliyojengwa kwa ufadhili wa kampuni ya Oilcom kwa ushirikiano na wananchi.*

*Waziri Mkuu amemaliza ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha Milkcom na Watercom kinachotengeneza Maji (Afya) na Maziwa (Dar Fresh)  kilichoko Kigamboni na kujionea uzalishaji huku akisisitiza kuwa serikali inachukua hatua za maksudi kuhakikisha Kigamboni kunakuwepo na umeme wa uhakika ili kuwezesha viwanda vilivyoko Wilayani humo vinazalisha bidhaa kwa wingi ili kutoa ajira zaidi na kulipa kodi serikalini.*

0 maoni:

Post a Comment